Na baada hapo, ukiongeza kelele zao, harufu yao…basi, utamleta mfanyakazi mzungu-mfaransa akaugua kichaa (Jacques Chirac)

Tarehe 19.01.1991, mjini Orléans (Ufaransa), bwana Jacques Chirac alikuwa akihutubia mkutano wa wanachama wa RPR (Rassemblement Pour la République), yeye akiwa mwenyekiti wa Chama hicho. Kwa kuwa alikuwa ameona kwamba Bw Jean-Marie Le Pen, kiongozi wa Chama « Front National » alikuwa na sifa nyingi kutokana na sera zake za chuki ya wageni, nae Chirac aliona bora kuonyesha kwamba siasa anayotaka kuifwata ni ya kulinda maslahi ya raia wafaransa wazungu. Kwa hio, aliwashangaza wadadisi wengi wa mambo ya siasa alipotamka : « Hatuwatupilii mbali wageni. Ila, kinachotukia sasa ni kwamba, kwa leo, wageni wapo wengi sana. Tatizo letu sio kuwa wao ni wageni ila, sasa, wamezidi kipimo »

Bila kutamka kinaganaga chuki dhidi ya wageni na hasa ubaguzi wa rangi, Chirac anaonekana hapa kwa sura yake ambayo huwa anaificha sana. Ni yeye pia ambae aliwahi kusema kwamba « Afrika haijaiva kwa Demokrasi ». Ila hapa, anaonyesha – kama ilivyo kawaida yake- kwamba aliyumba kisiasa na kiitikadi. Katika hotuba hio hio aliendelea akisema : »Mfanyakazi mzungu ambae anaishi La Goutte d’or, ambae anafanya kazi na mke wake, huku wakiwa na mshahara wa 15 000 FF, anapoona familia ya weusi, baba mmoja na mabibi watatu ao wanne, watoto pata ishirini (20) ambae anapokea msaada wa dhidi ya 50 000 FF, bila kufanya kazi yoyote ile…mfanyakazi mzungu huu hushikwa na bumbuwazi. Na baada hapo, ukiongeza kelele zao, harufu yao…basi, utamleta mfanyakazi mzungu-mfaransa akaugua kichaa… »

Kama ilivyo kila mara kwa Chirac, maneno yake hayana msimamo wowote kwani akiaga kitu si kweli kwamba atakiteleza. Anaweza kusema hiki leo, kesho akasema kinyume chake. Na hasa kuhusu matamshi haya, wadadisi wengi wa mambo ya siasa waliuliza kompyuta zote za Ufaransa ni mtu gani huyu, wa asili ya Afrika chini ya Sahara, ambae alipata kila mwezi msaada wa Franka elfu hamsini. Hakupatikana mtu yeyote…Ina maana, matamshi haya yalikuwa ya uchochezi tu .

Mfuasi mwingine wa Chirac, kwa jina la Robert Pandraud, akihojiwa na wanahabari kuhusu matamshi haya ya kushangaza, alisema : » Jee, ni ubaguzi kusema kwamba kuna tofauti ya harufu baina  mapishi ya kabichi na yale ya vitunguu swaumu ? » Ni dhahiri kwamba ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi, nchini Ufaransa, ni jambo la kawaida kwa watu wa mrengo wa kulia. Juzi hapa, hata msoshalisti, mkuu wa mkoa kusini magharibi mwa Ufaransa, amesema kwamba katika timu la taifa la mpira wa kandanda nchini Ufaransa, weusi ni wengi mno…Inaonekana kabisa kwamba ubaguzi wa rangi, kuwaonea weusi na waarabu, unaleta kuwanyima haki hata raia wafaransa wazaliwa nchini Ufaransa.

Kutokeana na matamshi haya, aliewahi kuwa Meya wa mji wa Lyon, Bw Michel Noir alisema : »Napendelea zaidi kupoteza kura katika uchaguzi kulikoni kupoteza moyo wangu »

Kilichoudhi sana waafrika wengi ni kwamba Bw Chirac amesema kwamba waafrika wana harufu mbaya, ina maana wananuka. Na wengi waliendelea kuonyesha kwamba Chirac, maishani mwake, hakukataa kupokea rushwa ao pesa zozote zile kutoka kwa viongozi kama Mobutu, Bongo, Houphouet Boigny…katika kampeni zake. Ila, kama alivyosema tokea enzi za kale, Bw Vespasianus, « pesa haina harufu »