Nukuu za siasa , uchumi na historia

Buhendwa eluga essy

 1. Lazma kiongozi ambaye anataka kudumu madarakani ajifunze kutoweza kuwa mwema

(Machiavel)

 1. Naamini kwamba iwapo ni kweli kwamba bahati nzuri hutuamulia nusu ya vitendo vyetu, lazma pia ituache wenyewe tuamulie nusu ingine (Machiavel)

 1. Hakuna nguvu wala mali bali watu  (Jean Bodin)

 1. Amueni kutotawaliwa  tena na mtakuwa huru (La Boétie)

 1. Inawezekanaje kuwa « mpersi » ? (Montesquieu)

 1. Mtu yeyote ambaye ana  madaraka, lazma huyatumia kinyume cha sheria (Montesquieu)

 1. Maandamano ambayo matukio yake ni kumung’oa mfalme  madarakani na kumnyonga ni kitendo ambacho ni cha kisheria kama kile kilichokuwa kikimleta yeye atoe hukumu la kifo ao la kunyang’anya mali ya wengine…(Jean-Jacques Rousseau)

 1. Yeyote atakaekataa kuheshimu matakwa ya jamii, atalazimishwa kuyashimu : hio haina maana ingine isipokuwa kuwa huru (Jean-Jacques Rousseau)

 1. Raia ana adui  mmoja tu : serikali yake (Saint-Just)

 1. Katiba iliyoumbwa kwa mataifa yote, haikuumbwa kwa taifa lolote (Joseph de Maistre)

 1. Bila ya kuyachukua madaraka, haiwezekani kuyatekeleza malengo . Ukiishajinyakulia madaraka, ni mara chache tu malengo hutekelezwa (Fidel Castro)

 1. Siasa haina nafasi darasani (Max Weber)

 1. Ulimwengu wa tatu upo, ila si rahisi (Yves Lacoste)

 1. Urusi ni kama mnyama mnono ambae aliyekuwa na njaa tokea muuda mrefu. Haiwezekani kumkataza kula (Winston Churchill)

 1. Algeria ni Ufaransa (François Mitterrand)

 1. Pesa haina harufu (Vespasien)

 1. Msanii maarufu gani Ulimwengu utapoteza ! (Néron)

 1. Haijawahi kutukia,  katika mambo ya vita, watu wengi wawe na deni kubwa kama hii  kwa watu wachache kama hawa (Churchill)

19. Hatutaenda Canossa (Bismarck)

 1. Ninafungua mashtaka (Emile Zola)

 2. Na kama ni mtu mmoja tu atakayebaki, huyo ni mimi (Victor Hugo)

 1. Nahisi : ni Dokta Livingstone ? (Stanley)

 1. Wewe pia, mwanangu ! (Juliasi Kaisari)

 1. Wamemuua Jaurès (Marguerite Poisson)

 1. Mimi ni mwenyeji wa Berlin (JF Kennedy)

 1. Kwa sasa hivi, tunajulikana zaidi kulikoni Yesu (John Lennon)

 1. Mke wa Kaizari lazma awe nje ya fununu yoyote ile (Juliasi Kaisari)

 1. Mimi sina hatia ya damu ya mtu huyu (Pilato)

 1. Nimekuja, nimeona, nimeshinda (Juliasi Kaisari)

 1. Ushindi mwingine mmoja kama huo, na basi, tutakuwa tumepotea (Pyrrhus)


 1. Lazma kiongozi ambaye anataka kudumu madarakani ajifunze kutoweza kuwa mwema (Machiavel)


Bwana Nicolo Machiavel (1469- 1527), mwanadiplomasia, mwenyeji wa Firenze (Italy), baada ya kujikuta bila kazi kulipotokea mageuzi nchini humo Italy, akaamua kuandika kitabu ili aweze kumshahuri yule ambaye yuko madarakani. Ndipo akaanza kuandika kitabu kiitwacho « Mtoto wa mfalme » (The prince ; le Prince). Katika kitabu hiki kilichoandikwa uhamishoni, Machiavel anataka kumshahuri yeyote yule ambaye ameingia madarakani namna ya kudumu madarakani, mbinu za kuongeza madaraka yake na jinsi ya kujikuta na sifa kubwa.

Tokea muuda mrefu sana, huko Ulaya, watu walifikiri kwamba kwa kufika madarakani, kwa kuongoza watu, lazma mtu awe mwema na mwenye akili timamu. Hayo yalikuwa maoni ya watu kama Marcus Tullius Cicero ila pia ya watu wengi ambao walifikiri kwamba kwa kuwa kiongozi lazma kupanga vizuri mambo ya uchumi wa nchi, kuwa mwenye sifa nzuri, mwenye mwenendo mzuri.

Machiavel, katika kitabu chake, anapinga maoni hayo. Anafikiri kwamba yeyote yule ambaye anataka kuwa kiongozi, lazma afikirie kila wakati kulinda na  kukuza madaraka yake. Ingekuwa watu wote ni wema, kiongozi yeyote yule angekuwa mwema. Ila, watu wote si wema, ao hasa, walio wengi ni wana roho mbaya, wana mbinu zao zinazowaleta watende mabaya, la sivyo, hawana maisha mazuri, hawaishi vizuri.

Kwa hio, bwana Machiavel anamshauri mtu yeyote anayetaka kutawala, kuwa na madaraka, kuwa kiongozi : « Yeyote yule anayetaka kuwa mwema, lazma aonekane vibaya kati ya wale wote walio wabaya. Lazma mtoto wa  mfalme ambaye anataka kudumu madarakani ajifunze kutoweza kuwa mwema »

Kwa maoni ya Machiavel, historia inatuonyesha kwamba kwa uchunguzi ya maisha ya wale waliopata madaraka makubwa, ni dhahiri kuona kwamba viongozi mashuhuri hawakuwa wala wema, wala wabaya. Kwa vyovyote vile, iliwabidi « wawe werevu kama sungura » na « wawe na  nguvu za simba » ; Machiavel, kwa hio anashahuri : »lazma ieleweke kwamba kuna namna mbili za kupigana vita : mojawapo  ni kutumia sheria, ingine ni kutumia nguvu. Namna hio ya kwanza (sheria) ni ile itumiwayo na binadamu ; hio ya pili inatumiwa na wanyama. Kufwatana na kwamba sheria haitoshi, lazma kutumia nguvu. Ni kwa hio, kiongozi, madarakani,  lazma atumie mchanganyo wa  utu na unyama. »

Maoni na fikra za Machiavel ni mambo ya mshikimshiki katika udadisi na utekelezaji wa siasa. Machiavel anataka kutuonyesha kwamba yeyote yule ambaye anataka kuwa na madaraka, kuwa kiongozi, sio lazma aonyeshe kwamba yeye ana sifa nzuri, ni mtu mwema, mstaarabu. La maana ni kutopoteza madaraka, kuendelea kukuza uwezo wake wa kumiliki mambo yote ambayo, kwa vyovyote, yakuze cheo chake. Kwa kutambulisha hio, Machiavel anatupa mfano wa Mfalme Kaisari Borgia ambae, kwa kuleta amani mkoani Romania, amemkabidhi madaraka mojawapo watu wake ambaye alikuwa na sifa ya kuwa mkorofi na jehuri. Yule mtu, kweli, kwa kutumia mabavu, akaleta mkoa huo upate amani na utulivu. Mara moja tu baada ya kurudishwa kwa amani na utulivu, Borgia akaomba mtu huyo afunguliwe mashtaka na kuhukumiwa kifo. Mwili wake ukakatwa vipande viwili, kuzunguushwa mjini na kuachwa hadharani .

Kwa hio, kwa maoni ya Machiavel, kiongozi hana sababu ya kujionyesha « mwema ». Mwandishi, mfalsafa Jean-Jacques Rousseau amesema kwamba Machiavel ni mtu mwema sana na lazma apewe sifa katika waandishi wote : « Kwa kutumia mbinu ya kumshauri mfalme ao kiongozi aingiae madarakani kwa madhumuni ya kumuonyesha namna ya kulinda maradaraka yake na kuyapa nguvu, Machiavel anatoa mashauri kwa  raia. »

Hata Baruch Spinoza ana maoni kama hayo ya Rousseau wakati anasema eti : « Huenda Machiavel anataka kuambia raia kwamba hakuna sababu ya kumkabidhi mtu mmoja madaraka yote, huku raia akifikiri kwamba usalama na uokovu wake unatokana na wema wa kiongozi…. »

Machiavel anajulikana sana ulimwenguni, hasa kwa yeyote yule ambaye anataka kuelewa siasa na mbinu zake. Msemwa wake ambao unajulikana zaidi ni ule ambamo anasema kwamba « nia yeyote ile inaruhusu njia yoyote ile » (la fin justifie les moyens). Ina maana kwamba katika mambo ya siasa, ukitaka kutekeleza lengo ao madhumuni fulani, huna budi kutumia mbinu zozote zile : uongo, wizi, ujanja, ragai…Ni kwa hio, wengine wanasema kwamba « penye nia, pana njia »….


 1. Naamini kwamba iwapo ni kweli kukubali kuwa bahati nzuri hutuamulia nusu ya vitendo vyetu, lazma pia ituache wenyewe tuamue kuhusu nusu nyingine (Machiavel)


Mara nyingi, Machiavel hakubaliani na fikra ao maoni ambayo yanavuma wakati wake. Tumeona jee amesema kwamba kiongozi hana sababu za kuwa mwema, kwani la mhimu ni kuongeza na kudumisha madaraka yake.

Katika nukuu hii, Machiavel anachungua jambo hili la bahati katika mambo ya binadamu. Namkumbuka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika tafsiri yake ya maandishi ya Shakespeare ambako anasema : « Mambo ya binadamu yana kujaa na kupwa ; Ukiyadaka yamejaa, huongoza ushindini ; Ukikosea, safari yote  ya maisha … ». Ni kusema kwamba maisha pia yanachukua sura ya « bahati nasibu », « lona », « libaku », « chance », « iragi », « lupemba »

Analotaka kusema Machiavel, ni kwamba maishani kuna bahati nzuri ambayo inaweza kukuleta ukapata nyadhifa, madaraka, raha, amani, fanaka, starehe….Ila, usije ukafikiria kwamba hio bahati itaendelea kukuletea kila la kheri. Lazma mwenyewe pia utumie mbinu zote ili maisha yasiwe tu ya kutegemea bahati nzuri. Wenyewe, lazma, tuweke mchango wetu katika kuboresha maisha yetu, kurekebisha pengamizi zote.

Enzi za Machiavel, kufwatana na imani ya kikristo na mafundisho ya wasomi wake, ilikua inakubalika kwamba « bahati » (fortuna) ndio ina amua maisha ya binadamu.  Kwa hio, lazma binadamu akubali ufukara ao utajiri wake kufwatana na kwamba hayo yote yameamuliwa na « bahati nzuri » ao « bahati mbaya »…

Machiavel anataka kumshahuri mtu yeyote kwamba bahati hukupa nusu ya fanaka ila nusu ingine, mwenyewe lazma ujitengenezee…Kwa hio, kutegemea bahati ni ujinga. Lazma kutumia mbinu zote ili kutekeleza maazimio tuliyojiwekea. Kwa hio, Machiavel anasema : « Nafahamu vizuri kwamba kuna watu ambao wanafikiri kwamba mambo ya Ulimwengu huu yanaongozwa na « Mungu» ao na « Bahati », kiasi ambacho hakuna mtu ambaye anaweza kupinga wala kuganga ujinga huo. Kwa hio, kila mtu anafikiri kwamba hakuna sababu ya kutoa jasho katika jitihada la kuwaleta walio wengi kutambua ujinga uliopo wa kufikiri mambo kama haya… Ili « uamzi-huru » (libre-arbitre) wetu usijikute katika hali mbaya, naamini kwamba iwapo ni kweli kukubali kuwa « bahati nzuri » hutuamulia nusu ya vitendo vyetu, lazma pia ituache wenyewe tuamue kuhusu nusu nyingine »

Katika kitabu chake « Hotuba kuhusu miaka kumi ya kwanza ya Tite-Live » ao « Discours sur la première décade de Tite-Live », Machiavel anaongea kuhusu sababu za sifa nzuri ya Wafalme ao Viongozi wa Roma. Anafikiri kwamba umashuhuri wao haukutokana na bahati nzuri bali na  ubora wa majeshi na mbinu za siasa  zao. Pamoja na kwamba watu wa Roma ya kale waliabudu « Miungu » kibao, walikua na siasa ya « KUJITEGEMEA ». Hapo, Machiavel anaamini kwamba haiwezekani kupinga « bahati » ila lazma wenyewe tuchungue ubaya na uzuri wake : « Nasema tena kwamba ni ukweli ambao hauna ubishi na ambao hauna sababu zakuletewa ushahidi popote pale katika historia, kwamba watu wanaweza kusaidia bahati, sio kuipinga, kusaidia kusuka nyuzi ziletazo bahati, sio kuzikata. Sina imani kwamba lazma mtu akae akisubiri bahati nzuri. Binadamu hawajui bahati ina nia ao madhumuni gani. Na kufwatana na kwamba « bahati » hutumia njia na mbinu zisizojulikana na mara nyingi kutotambulika, binadamu huwa wanakaa tu na matumaini, mategemeo… »

Kwa kuonyesha kwamba  bahati nzuri haiji bila kuibunia mipango, Machiavel anaongeza akisema kwamba yeye analinganisha bahati na mito : «  Nalinganisha bahati na mojawapo mito ambayo inapojaa, inakasirika na kuleta mafuriko katika bonde zote kando yake, ikibomoa nyumba  na miti kando yake. Mito hio, inapobomoa udongo upande huu, huupeleka upande mwingine…Kila anayeona mafuriko kama haya, hukimbia , bila kufikiria kwamba anaweza kujenga ukuta ili mafuriko yasimletee hasara…Bahati nayo huchukua njia kama hizi, hutumia mbinu kama hizi : bahati hutokea mahala ambapo inajua kwamba hakuna nguvu yoyote ya kuipinga ao ya kuizuia »

Lazma kubuni mipango ili bahati itokee. Lazma kufikiria mambo ili yatokee. Yeyote yule anaekaa, tokea asubuhi hadi jioni, ao anayepitisha wakati wake katika anasa za dunia, ataiona bahati ikiwaendea wale wenzake ambao wanaichokoza bahati, ambao wanajitahidi kutoa maisha yao katika hali ya dhiki na kuyapeleka, kwa njia zozote zile, katika hali ya neema. Bahati ni kama kilimo : kwa kuvuna lazma uwe umepanda.

Machiavel anaamini kwamba jamii yoyote ile (kabila, taifa, mkoa, wilaya, kijiji, mtaa) inategemea hali ya watu ambao ni wenyeji wake. Iwapo wana nia ya kuleta maendeleo na wakitia bidii, maendeleo yanakuja. Wakiamua kuwa wajanja, wavivu, wapenda starehe, watajikuta wanashindwa na kuboresha hali na mali zao.

Katika mambo ya siasa, lazma kuamua na kutekeleza. Kubuni mambo yote kichwani na kutoshiriki huleta hasara kwa mwanasiasa ao kwa jamii nzima. Kusubiri wakati mzuri, kutegemea bahati nzuri, si kitu kizuri kwa mtu yeyote yule ao jamii yeyote ile. Lazma kuelewa hali halisi na kutoa maswali kwa maswala yaliyopo wakati huo huo…Kusubiri bahati nzuri ni kuamua kutotenda, ni kupendelea kuswali kuliko kutatua matatizo.

3- Hakuna nguvu wala mali bila watu (Jean Bodin)

Mara nyingi, historia hutuonyesha miujiza yake na kutupa pia mafundisho mengi kuhusu sifa za watu ambao wana sifa zao. Jamaa huu, Jean Bodin (1530-1596), ambae ameandika vitabu vingi, kanukuliwa na wataalam wengi, na wadadisi kibao kama Montesquieu, Rousseau, John Locke….anajulikana  hivi sasa kutokana na sentensi hii : « Hakuna nguvu wala mali bila watu »  Ina maana kwamba, katika eneo la utawala wowote, ni watu ndio msingi wa maendeleo, sio mali ambazo watu binafsi wanazo ao nguvu za silaha za majeshi.

Nukuu hii, tunaipata katika  kitabu chaka «  Les six livres de la République » (Vitabu sita vya Jamhuri). Katika kibabu hiki, Jean Bodin, anataka kuonya kuhusu hatari ya kuwepo, katika Jamhuri ao tawala lolote, kwa watu ambao ni matajiri wakubwa na wengine ambao hali yao ya ufukara inatisha. Kwa hio, Bwana Jean Bodin anasema : « Kwa vyovyote vile, hakuna sababu ya kuogopa kuwepo kwa watu wengi katika tawala lolote ao Jamhuri yoyote ; kufwatana na kwamba, hakuna nguvu wala mali bila watu…Kuwepo kwa watu wengi kunakinga tishio la mkiki mkiki wa siasa…Ni hatari kubwa kuona Jamhuri inagawanyika katika tabaka mbili : tajiri na fukara. Hio hutukia mara nyingi katika tawala ao Jamhuri ambamo watu si wengi. »

4-Amueni kutonyanyaswa na mtakuwa huru

Etienne de la Boétie (1530-1563), katika kitabu chake « Hotuba kuhusu kunyanyaswa kwa hiari » (Discours de la Servitude volontaire) anazusha hapa swali la maana katika mambo ya siasa : inatokana na nini watu wengi wakubali kunyanyaswa na mtu mmoja ? Kwa nini watu wengi wanajikuta wakikubali kunyimwa haki na uhuru wao na kukubali kuheshimu amri itokayo kwa mtu mmoja ?

Jibu kwa swali hilo tunalipata katika kijitabu chake kilichopigwa chapa baada ya kifo cha bwana La Boétie na jibu lenyewe ni hili : raia akikubali kunyanyaswa ni kwani anakubali kwa hiari. Hali yake ya utumwa, hali yake ya utwana, haitokani na nguvu ao mali za yule « bwana », ila kwa udhaifu wake. Nduli hustawi tu wakati raia hujiuzulu.

Etienne de la Boétie, nje ya mambo ya siasa, anajulikana pia kwa kuwa ametunga msemwa mzuri kuhusu urafiki. Akiongea kuhusu urafiki wake na Montaigne, mwandishi maarufu huko Ufaransa karne tano zilizopita, La Boétie aliwahi kusema  kwamba urafiki wake na Montaigne unaeleweka tu « kwani ni yeye, kwani ni mimi ». Hapa majuzi, bwana Laurent Fabius,  waziri mku wa rais François Mitterand, kwa kuonyesha kwamba hakukubaliana na rais kwa kumpokea rais wa Poland, dikteta Jaruzelski akiwa safarini Ufaransa na kupokelewa kwa shangwe, alisema kwamba, hakubaliani, kufwatana na kwamba « yeye ni yeye, mimi ni mimi ».

Bwana Montaigne, baada ya kifo cha rafiki yake, akapigisha chapa maandishi ya La Boétie kwani enzi hizo kulikuwepo na mgongano wa kidini kati ya Waprotestanti na Wakatoliki unaojulikana kwa jina la « vita vya kidini » (guerre des religions). Akakusanya kurasa pata arubaini na maandishi hayo akayapa kichwa cha habari ifwatayo « Contre un » (Against one).

Maoni na hasa pendekezo la Etienne de la Boétie linatokana na kuwa haiwezekani ujitambue binadamu bila kuwa mtu huru : ubinadamu ni uhuru. Kama binadamu hakupata elimu potovu, haiwezekani akubali kunyanyaswa, kuonewa , kunyonywa. Uhuru ndio lengo la jamii lolote lile, la mtu yeyote yule. Kutokuwa huru ni kama kuwa mnyama wa porini.

Ila, hapa sasa ndipo Etienne de la Boétie anajiuliza : inakuwaje watu ambao ni wengi sana katika jamii lolote lile wanaukubali utumwa, utwana ? Na jibu ambalo analipata haraka ni kusema kwamba hapo walio wengi wanaukubali utwana wa hiari (servitude volontaire) : « Hapa ndipo ningependelea kuelewa kwa nini inawezekana watu kadhaa miji kadhaa mataifa kadhaa, wanamvumilia nduli mmoja tu ambae nguvu pekee anayo ni ya kuwakera tu …Wala nduli huyo hana uwezo wa kuwatendea mabaya isipokuwa wanayakubali, wasipopendelea kumvumilia kulikoni kumpinga… »

Katika historia  ya fikra za siasa, Etienne de la Boétie ni mtu ambaye ni maarufu sana kwani, kama Machiavel, Rousseau na Marx, anaonyesha kwamba kutawaliwa, kunyanyaswa kunaanza kichwani, rohoni , kiakili. Mtawala anatulazimisha kutekeleza matakwa yake kwani tu sisi tunakubali. Sio eti ni kwani yeye ana akili ao ujuzi maalum. Tunakubali kutawaliwa na kukubali huko kunatokana na udhaifu wetu, sio eti kukubali kutekeleza amri za mtawala kunatokana akili ao nguvu zake. Sisi wenyewe tunachangia kukandamizwa, kunyanyaswa, kunyonywa, kuonewa.

La Boétie anaonyesha dhahiri kwamba kutawaliwa katika hali ya kunyanyaswa kunatokana na kuwa kuna watu wachache ambao wanajikuta wakimbembeleza mtawala, wakimuambia maneno matamu, wakimtukuza. Na huyu akaamini kwamba kweli yeye ni maarufu kiasi kutokana na sifa anazopewa na hawa wachache anafikiri kwamba jamii nzima inamsifu, inampenda, inamchukua kama « Mungu ». La Boétie anaonyesha jambo hili anaposema : » Kila mara, huwa kuna watu wanne, watano, ambao wanasikilizwa sana na NDULI kwa kuwa wamejipendekeza ao kwa kuwa mwenyewe amewaita ili wachangie naye unyama wake,  washiriki wa raha zake, watekelezaji wa amri zake, waporaji mali wenziwe…Hao watu sita humtayarisha vizuri huyu mtawala kiasi lazma aonekane mkali kwa jamii…Hawa watu sita wanao pia mia sita ambao wanakula kwa jina la hawa sita wa mwanzoni…Hawa mia sita nao wanao chini yao elfu sita ambao wanapewa maradaraka ua kuongoza mikowa, wilaya, vijiji…Kwa hio, inaonekana kwamba ukianzia chini, ukianza kuvuta nyavu yenyewe ambamo wote wanashikwa, utaona kwamba sio watu elfu sita, ila milioni sita …ambao wote wako chini ya uamzi na matakwa ya Nduli… »

Inaonekana kwamba chini ya uongozi wa Nduli, kila mtu naye hujikuta  nduli mdogo pale alipo.

Baada ya kuonyesha kwamba kunyanyaswa na watawala kunatokana na kukubali kwa watawaliwa, La Boétie anataka watu wapinge kunyanyaswa, kuonewa, kunyonywa. Lazma kuipinga serikali ambayo inatunyanyasa.

La Boétie anaomba watawaliwa wanaonyanyaswa wasifikiri kwamba anayewanyanyasa ni mtu tofauti ao mtu maalum ambae ana kipaji tofauti. Madaraka yake hakuyapewa na Mwenyezi Mungu. Wakitaka kutoka katika hali ya utwana, lazma wapuuze ubwana wa nduli yule na wafwasi wake ambao, wote, wanajali maslahi yao kwanza. Kwa jumla, kufwatana na maoni ya La Boétie, kuwa huru ni kutaka kuwa huru.

5- Inawezekanaje kuwa « mpersi » ? (Montesquieu)

Mtaalam ya mambo ya sheria, bwana Montesquieu, ana sifa nzuri kwa kuwa ni mtu ambaye ameonyesha kwamba katika Jamhuri, lazma madaraka yawekewe mipaka. Amependekeza kuwepo na watu ambao wanatunga sheria, wengine watekeleze madhumuni ya jamii kufwatana na taratibu za sheria, na wengine wawe na madaraka ya kuamua.

Katika nukuu hapa juu, Montesquieu anatoa hadithi kuhusu watu wa Iran ambao walikuja kutembelea mji wa Paris mwaka 1712. Watu hao walipokuwa wakipita barabarani, wenyeji wa Paris walikuwa wakija dirishani na kushangaa sana kuona watu hawa ambao, kwa mavazi na kwa mwendo wao, walikuwa tofauti kabisa na wanachokifahamu kwao. Na wenyeji hawa wa Paris, walikuwa wakijiuliza : « inawezekana je kuwa mpersi ? »

Hapa, bwana Montesquieu anataka kuonya jamii yoyote ile na kuishahuri kuachana na tabia mbaya ya kufikiri kwamba chochote kile kizuri, lazma kiwe kitu ambacho ni cha kwetu. Jamii zote zina mema na kasoro, zina hali ya neema na hali ya dhiki. Kuchukua jamii lake kama ndilo bora zaidi (ethnocentrism) ni namna fulani ya kufikiri kwamba kuna rangi bora kulikoni ingine, kuna kabila bora kulikoni ingine, kula taifa bora kulikoni ingine, kuna dini bora kuliko ingine. Hapa ndipo kunaanza ubaguzi wa rangi, wa kabila, wa dini. Na pia ni chanzo cha kutoelewa kwamba kila kitu ni kizuri pale kilipo wala  si mshangao kuona kitu tofauti na kile tunachozoea kukiona.

Montesquieu anaonyesha kwamba hakuna haja kujilimbikizia ukoo, taifa, kabila, dini, rangi. Si vizuri kutoa uamzi kwamba kabila fulani, rangi fulani, taifa fulani, dini fulani ni bora, ni nzuri, ni kubwa, ni ya kuridhisha kulikoni nyingine. Kutokana na utamaduni wa jamii fulani, haiwezekani kusema kwamba utamaduni wowote usiofanana haufai.

Lazma kukubali kwamba kuwa tofauti sio kuwa mzuri ao mbaya, mkubwa ao mdogo. Lazma tuepuke « kitanda cha Prokusti ». Prokusti ni shujaa ambae, katika historia za Wagiriki wa zamani, alikuwa na kitanda chake ambako alikuwa akikaribisha wageni. Ukiwa mrefu kulikoni kitanda chake, anakukata miguu na kichwa hadi ulingane na kitanda chake ; ukiwa mfupi kulikoni kitanda chake, anavuta miguu na kichwa hadi ufikie urefu wa kitanda chake.

Montesquieu anafundisha uvumilivu na uwastani. Anaomba kila jamii itunge sheria ambazo zinaambatana na utamaduni, desturi na mila zake. Hakuna haja kufikiri kwamba sheria za jamii fulani, lazma ziwaongoze watu wa jamii nyingine zote. Kila mahala na mila zake, kila mila na sheria zake, bila kufikiria kwamba kuna sheria ambayo lazma, popote pale, lazma iwe na uzito ule ule kama mahala ilipoanzishwa. Kila jamii inatunga sheria kwa maslahi yake, na maslahi yake sio maslahi ya kila jamii ulimwenguni.

6- Mtu yeyote ambae ana madaraka, lazma huyatumia kinyume cha sheria (Montesquieu)

Kwa maoni ya Montesquieu, kuwa mtu huru ni kuwa na uhakika kwamba huhukumiwi na mtu, hulazimishwi kutekeleza matakwa yoyote ya yeyote ule. Taifa ambalo linahakikisha uhuru wa raia ni lile ambalo linawalinda wazalendo wake dhidi ya kuonewa, kunyang’anywa : « Na mtu ni huru iwapo anaamini kwamba hasira ao chuki za mtu yeyote yule haziwezi kumuondoa maisha ao mali yake »1 . Uhuru ni imani kwamba kuna usalama wa hali na mali. Kwa hio, uhuru ni imani. Uhuru ni kujisikia kuwa katika hali ya usalama, wakati wowote ule, mahala popote pale.

Anapoongea kuhusu « uhuru », Montesquieu anatumia ujuzi, ufahamu anao kutokana na kwamba alikuwa na umri wa miaka ishirini na sita, mfalme Louis XIV (mfalme-jua), alipofariki dunia. Mfalme huyu wa Ufaransa ameufanya utawala wake kugeuka wa kidikteta.

Kwa kuwa familia ya Montesquieu ilikua na imani ya kiprotestanti na ikalazimishwa kujiunga na imani ya kikatoliki kwa sababu za vita vya kidini, Montesquieu anataka kuonyesha kwamba mfalme huyu ambae alitakiwa kulinda hali na mali za watu wake, alijikuta akiwanyanyasa watu wake na kuwanyang’anya mali zao ao kuwaondoa maisha yao kwa kuwa wao ni « waprotestanti ».

Kitabu « L’Esprit des lois » (moyo wa sheria) kimeandikwa ili utawala wa Ufaransa usijikute katika hali ya kidikteta. Kwa hio, swali lililopo ni kutumia mbinu gani ili utawala usigeuke wa kidikteta ? Na Montesquieu anapendekeza kwamba kwa kuwa na uhakika kwamba yeyote yule anae madaraka hatayatumia kinyume cha sheria na kujikuta amegeuka « nduli », lazma madaraka yake yapewe mipaka. Lazma madaraka yoyote yawe na mipaka ambayo ni madaraka wanao watu wengi. Lazma madaraka yazuie madaraka, lazma madaraka yazuwiliwe na madaraka.

Montesquieu anahimiza kwamba lazma kuwepo « ugawaji wa madaraka » (distribution des pouvoirs), na hasa « utenganaji wa madaraka » (séparation des pouvoirs). Montesquieu anataka madaraka yapewe mipaka, na mipaka hiyo yanaweza yakatokea katika desturi na mila za watu, ao imani zao za kidini. Lazma mipaka ya madaraka iwe imeandikwa rasmi katika katiba.

Kwa hio, Montesquieu anatambua aina tatu za  madaraka :

 • Madaraka ya kutunga sheria

 • Madaraka ya kutekeleza malengo ya kisiasa

 • Madaraka ya kutoa uamzi yatokeyapo malumbano

 

7-Maandamano ambayo matukio yake ni kumung’oa mfalme  madarakani na kumnyonga ni kitendo ambacho ni cha kisheria kama kile kilichokuwa kikimleta yeye atoe hukumu la kifo ao la kunyang’anya mali ya wengine (Jean-Jacques Rousseau)

Rousseau ni mdadisi maarufu wa mambo ya siasa, kiasi ambacho tunaweza kusema kwamba, kwa fikra na maoni yake amewaleta  wazalendo wakaamini kwamba ni watu huru na uhuru wake una mipaka yake katika uhuru wa watu wengine.

Rousseau anataka binadamu yeyote yule katika jamii fulani ajitambue kama mtu anayejiamulia mambo yake ila akubali kujiweka chini ya uamzi wa walio wengi.

Rousseau anahimiza kwamba mwenye madaraka hayapewi na Mungu, bali na watu. Kwa maoni ya Rousseau, madaraka hayatoki kwa Mungu, kuelekea kwa mfalme na baadae mfalme ayakabidhi kwa walio chini ya ulinzi wake. Rousseau anakanusha maoni hayo na anasema, kinaganaga, kwamba ni raia ndio wanamkabidhi mfalme madaraka, kwa manufaa yao.

Rousseau amejikuta na sifa kubwa akiwa na umri wa miaka thelathini na nane (38), alipotoa kitabu chake « Hotuba kuhusu sayansi na sanaa » (Discours sur les sciences et les arts). Maandishi haya yalizusha mshangao na masikitiko ulaya nzima kwa kuwa Rousseau anakanusha maoni yaliyokubaliwa hadi hapo. Ilikuwa imekubaliwa, hadi hapo, kwamba maendeleo katika fani za elimu na teknolojia yalileta, kwa vyovyote vile, uboreshaji wa hali ya maisha : maendeleo yalileta fahari, raha, maisha mazuri. Rousseau alisema kinyume cha maoni hayo : binadamu huzaliwa mwema, maisha katika jamii humgeuza mtu mbaya na hawezi kufikia hali ya fahari, hali ya raha.

 1. Yeyote atakaekataa kuheshimu matakwa ya jamii, atalazimishwa kuyaheshimu : hio haina maana ingine isipokuwa kuwa huru (Jean-Jacques Rousseau)

 1. Raia ana adui  mmoja tu : serikali yake (Saint-Just)

1 Mes pensées (XXII)